Mapema hii leo Jumapili 20 Februari, viongozi wa kusini Australia, walianza kampeni za uchaguzi kwa kina katika siku ya kwanza rasmi ya kampeni za uchaguzi wa jimbo hilo. Gavana wa Kusini Australia Frances Adamson, alitoa hati iliyo tangaza tarehe ya uchaguzi jana hatua ambayo ilianzisha kampeni zitakazo dumu kwa wiki nne hadi siku ya uchaguzi tarehe 19 Machi.
Katibu Mkuu wa jumuiya ya kujihami NATO, Jens Stoltenberg, ameliambia shirika la utangazaji la umma nchini Ujerumani, ARD siku ya Jumamosi, kwamba ishara zote zinaonesha Urusi inapanga shambulio kamili dhidi ya Ukraine. Pamoja na hayo, Stoltenberg alisema NATO bado ina dhamira ya kutafuta suluhisho la kisiasa. "Tunaitaka Urusi ibadili mkondo na kukaa chini nasi," alisema.
Ethiopia leo itaanza kufua umeme kutoka kwenye bwawa lake la The Grand Ethiopian Renaissance linalokabiliwa na utata lililoko katika mto Nile. Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya nchi hiyo. Bwawa hilo limekuwa chanzo kikuu cha mzozo wa kikanda tangu kuanza kwa ujenzi wake muongo mmoja uliopita. Mataifa jirani ya Ethiopia, Misri na Sudan, yanasema bwawa hilo ni kitisho kwao kutokana na utegemezi wao wa mto Nile huku Ethiopia ikisema mradi huo ni muhimu kwa ajili ya usambazaji wa umeme na maendeleo.