Jeshi la Polisi la Victoria linatarajiwa kumtafuta kiongozi mpya, baada ya kamishna wake Shane Patton kujiuzulu. Kamishna Patton amesema ali ishauri serikali ya Victoria jana Jumapili, kuwa ame amua kujiuzulu kutoka wadhifa huo mara moja. Hatua hiyo imejiri baada ya asilimia kubwa ya nguvu kazi yake, kutangaza kutokuwa na imani kwa uongozi wake.
Bodi ya Benki Kuu imefanya mkutano wa kwanza asubuhi ya leo 17 Februari, ambapo wanachama wa bodi hiyo wata shiriki katika mkutano wa kwanza wa siku mbili mwaka huu, kufanya maamuzi kuhusu viwango vya riba. Kiwango rasmi cha hela taslim kimekuwa katika kiwango cha juu kwa muda wa miaka 13 ambacho ni asilimia 4.35 tangu Novemba 2023.
Mke wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda aliye chini ya ulinzi Kizza Besigye, Jumapili amesema ana wasiwasi kuhusu afya yake, ikiwa karibu wiki moja baada ya mgombea huyo wa zamani wa urais kuanza mgomo wa kula. Katika kesi ya kutishia usalama wa taifa, Besigye aligoma kula kuanzia Februari 10 akipinga kuzuiliwa kwake, huku wakili wake akimuelezea kuwa mgonjwa sana.
Umoja wa Afrika umeonya dhidi ya kugawika kwa taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, siku mbili baada ya waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa M23 kudhibiti mji wa pili kwa ukubwa nchini humo wa Bukavu. Waasi hao tayari wanaudhibiti mji wa Goma waliouteka mwishoni mwa mwezi Januari. Mapigano yanayoendelea Kongo yameyatia wasiwasi mataifa jirani na yale ya Magharibi kuhusu kutanuka kwa mzozo huo.